Zaburi 5

Zaburi 5
Sala Kwa Ajili Ya Ulinzi Wakati Wa Hatari
Kwa mwimbishaji. Kwa filimbi. Zaburi ya Daudi.
1 Ee Bwana, tegea sikio maneno yangu,
uangalie kupiga kite kwangu.
2 Sikiliza kilio changu ili unisaidie,
Mfalme wangu na Mungu wangu,
kwa maana kwako ninaomba.
3 Asubuhi, unasikia sauti yangu, Ee Bwana;
asubuhi naleta haja zangu mbele zako,
na kusubiri kwa matumaini.
 
4 Wewe si Mungu unayefurahia uovu,
kwako mtu mwovu hataishi.
5 Wenye kiburi hawawezi kusimama mbele yako,
unawachukia wote watendao mabaya.
6 Unawaangamiza wasemao uongo.
Bwana huwachukia
wamwagao damu na wadanganyifu.
 
7 Lakini mimi, kwa rehema zako kuu,
nitakuja katika nyumba yako,
kwa unyenyekevu, nitasujudu
kuelekea Hekalu lako takatifu.
8 Niongoze katika haki yako, Ee Bwana,
kwa sababu ya adui zangu,
nyoosha njia yako mbele yangu.
 
9 Hakuna neno kinywani mwao linaloweza kuaminika,
mioyo yao imejaa maangamizi.
Koo lao ni kaburi lililo wazi,
kwa ndimi zao, wao hunena udanganyifu.
10 Uwatangaze kuwa wenye hatia, Ee Mungu!
Hila zao ziwe anguko lao wenyewe.
Wafukuzie mbali kwa sababu ya dhambi zao nyingi,
kwa kuwa wamekuasi wewe.
 
11 Lakini wote wakimbiliao kwako na wafurahi,
waimbe kwa shangwe daima.
Ueneze ulinzi wako juu yao,
ili wale wapendao jina lako
wapate kukushangilia.
12 Kwa hakika, Ee Bwana, unawabariki wenye haki,
unawazunguka kwa wema wako kama ngao.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc.
Scripture text reproduced under Creative Commons Attribution–ShareAlike 4.0. Original Scripture wording is unchanged; navigation and presentation are adapted under the same license. Original edition: Read on eBible.org. Full edition and license information.